Taarifa kwa vyombo vya Habari
Chanzo: LEIBNIZ INSTITUTE FOR ZOO AND WILDLIFE RESEARCH
Dar es Salaam| 24-FEB-2024. Fisi wenye madoadoa wanakabiliwa na hatari katika Hifadhi ya Serengeti. Watafiti kutoka Taasisi ya Leibniz ya Utafiti wa Wanyama na Wanyamapori walichambua takwimu za miongo mitatu, na kubainisha sababu kadhaa za vifo vya fisi barabarani kutokana na kugongwa na vyombo vya moto. Uchunguzi huu wa muda mrefu umegundua vihatarishi vikuu zaidi ya vile vilivyotarajiwa. Awali, ilidhaniwa kuwa idadi ya watalii wanaoingia ndani ya hifadhi ni sababu kubwa. Fuatilia kwa undani habari hii ili kufahamu ni mambo gani hatarishi yanaweza kuchangia wanyamapori kugongwa na magari hadi kufa katika Hifadhi ya Serengeti.
Kwa zaidi ya miongo mitatu, watafiti wamekuwa wakitafuta majibu kuhusu suala hili. Yafuatayo ni matokeo ya utafiti wao.
Hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania ni makao ya idadi kubwa ya wanyamapori, ikiwa ni pamoja na fisi wenye madoadoa au wakifahamika kama Crocuta crocuta kwa jina la kisayansi. Licha ya shughuli nyingi za binadamu kupigwa marufuku katika hifadhi hii, magari hurusiwa kuendeshwa kupita ndani ya eneo hilo lililohifadhiwa.
Kwa kutumia mkusanyiko wa takwimu za miaka 34, timu ya wanasayansi kutoka Taasisi ya Leibniz ya Utafiti wa Wanyamapori na Bustani za wanyama au Zoo (Leibniz-IZW) walichambua mambo yaliyochangia fisi kugongwa na magari hadi kufa. Kwanza kabisa, ni aina ya barabara, na pili, uhamaji wa kila mwaka wa makundi makubwa ya wanyama walao majani katika hifadhi ya Serengeti na mabadiliko ya msimu ya maeneo ya wanyama wanaowindwa na fisi wenye madoadoa.
Matokeo haya yalichapishwa katika jarida la kisayansi la hifadhi zakibaiolojia, linaloitwa Biological Conservation. Yanatoa ufahamu mpya kuhusu mambo yakiikolojia na kitabia yanayowaweka wanyama wanaokula wanyama wengine, katika hatari ya kufa kutokana na kugongana na magari.
Duniani kote, wanyamapori wengi huuliwa kwa kugongwa na magari, hata katika maeneo yaliyohifadhiwa. Athari hizi za barabarani zinazidi kuongezeka kutokana na ukuaji wa idadi ya watu wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa na kuongezeka kwa utalii wa wanyamapori. Hata hivyo, kulikuwa na ufamamu mdogo kuhusu mambo yanayosababisha uwepo wa matukio ya wanyamapori hao kugongwa na magari hadi kufa.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeunganishwa na mtandao wa barabara. Barabara kuu ni za changarawe zilizofunikwa na murram ambazo hutumiwa sio tu na magari ya watalii, malori ya kusafirisha vitu katika kambi za watalii, wafanyakazi wa hifadhi na wanasayansi, bali pia na magari yanayopita huko kama vile malori na mabasi yanayosafiri nchi nzima mwaka mzima. Mbali na hayo, kuna njia nyingi zisizo na lami za uangalizi wa wanyamapori zinazofika hadi kwenye kambi za watalii. Kama sehemu ya utafiti huu wa muda mrefu katika Hifadhi ya Serengeti kati ya 1989 na 2023, wanasayansi wa Leibniz-IZW walibaini fisi wenye madoadoa 104 waliokuwa wamegongwa na gari. Wanasayansi hao walitumia visa hivi kuchunguza mambo ya kimazingira na muda yaliyochangia fisi hawa wenye madoadoa kugongwa na kuuawa na magari, na kuchunguza ni kwa kiasi gani fisi wa kundi fulani la umri, jinsia au cheo cha kijamii waliathiriwa.
Katika uchunguzi huu, vipengele viwili vilionekana kuwa vya muhimu sana. Kwanza kabisa, fisi waligongwa zaidi kwenye barabara kuu kuliko njia ndogo; huenda ni kwasababu magari hupita kwa kasi zaidi barabara kuu na magari yanayopita huko huwa ni mengi. Pili, muda na eneo la ajali viliendana na matukio ya uhamaji wa msimu wa makundi makubwa ya wanyama walao nyasi (nyumbu, pundamilia na swala wa Thomson), ambao ndio mawindo makuu ya fisi wenye madoadoa katika hifadhi ya Serengeti. Matokeo haya yanaakisi tafiti nyingine zilizoonyesha kuwa hatari ya kugongwa na gari hadi kufa huongezeka sambamba na uhamaji wa wanyama na umbali ambao wanyama hao hutembea. Mbali na hayo, fisi waliogongwa walipatikana karibu sana na vyanzo vya maji na makazi ya watu, mahali ambapo inadhaniwa fisi hawa huvutiwa na uwepo wa masalia ya chakula cha binadamu.
“Kinyume na matarajio, mabadiliko yakimsimu ya idadi ya watalii katika ukanda huo hayakuonekana kuathiri kiwango cha vifo vya wanyama hao,” anasema Marwan Naciri, ambaye alijiunga na Leibniz-IZW kwa ajili ya mradi huu na ndiye mtafiti kiongozi na mwandishi mkuu wa chapisho hili.
Sehemu ya kipekee ya takwimu zilizotumika ni kwamba baadhi ya fisi waliogongwa na magari walikuwa wanajulikana mmoja mmoja, hivyo basi historia ya maisha yao iliweza kuchunguzwa. Matokeo yalionyesha kuwa fisi wazima wakike walikuwa wanagongwa zaidi, labda kwa sababu wanatembea umbali mrefu zaidi, kwani wao ndiyo hutembea mara kwa mara kati ya mapango ya pamoja na wanyama wanaoohama ili kusaka chakula karibu na wanyama hao na kuwatunza watoto.
Sarah Benhaiem, Mtafiti kutoka Taasisi ya Leibniz-IZW na Kiongozi mwenza wa Mradi wa Fisi wa Serengeti(Serengeti Hyena Project), anasema: “Kama tulivyogundua katika utafiti wa awali, majeraha yanayosababishwa na mitego haramu ya waya yanaathiri hasa fisi wazima majike.”
Vifo vya barabarani na mitego ni visababishi muhimu vya kuzingatia kuhusu vifo vya fisi wazima katika eneo la Serengeti.
Mtafiti mwenza, Sonja Metzger, ambaye pia ni kiongozi mwenza wa Mradi wa Fisi wa Serenget(Serengeti Hyena Project), anaongeza: “Bado haijabainika iwapo vifo hivi vinavyoathiri zaidi fisi wazima wa majike vinatishia ustawi wa spishi ya fisi wenye madoadoa katika hifadhi ya Serengeti.”
Mtandao wa barabara unatarajiwa kupanuka siku za usoni. Ufahamu wa mambo yanayosababisha magari kugongana na wanayamapori hadi kufa,utasaidia katika kubuni hatua madhubuti za kupunguza madhara.
Katika hifadhi ya Serengeti, hatua hizi huenda zikajumuisha ufuatiliaji bora wa mwendo wa magari, hasa kikomo cha kasi cha kilomita 50 kwa saa, udhibiti mkali wa marufuku ya kuendesha magari usiku na ukomo wa idadi ya magari katika barabara kuu. Upangaji mzuri wa ujenzi wa barabara na utekelezaji wa hatua za kupunguza madhara ni muhimu ili kuhakikisha uendelevu wa uhifadhi wa wanyamapori katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Jinsi ya kupata utafiti huu:
Naciri M, Planillo A, Gicquel M, East ML, Hofer H, Metzger S, Benhaiem S (2023): Miongo mitatu ya matukio ya wanyamapori kugongana na magari katika eneo lililohifadhiwa: Barabara kuu na safari ndefu za kuelekea wanyama wanaoohama zinaongeza vifo vya barabarani vya fisi wenye madoadoa Serengeti. ( Jarida la Biological Conservation) 279, https://doi.org/10.1016/j.biocon.2023.109950.
Benhaiem S, Kaidatzi S, Hofer H, East ML (2023): Gharama za uzazi wa muda mrefu zitokanazo na majeraha ya mitego kwa spishi muhimu za wanyama wanaokamatwa bila kukusudiwa kwenye nchi kavu. Jarida la Animal Conservation 26, 61-71 https://doi.org/10.1111/acv.12798.
Kwa mawasiliano zaidi:
Leibniz Institute for Zoo and Wildlife Research (Leibniz-IZW)
in the Forschungsverbund Berlin e.V.
Alfred-Kowalke-Str. 17, 10315 Berlin
Dr. Sarah Benhaiem (German, English and French)
Scientist Dept. Ecological Dynamics
Tel.: +49 30 5168-466
E-Mail: benhaiem@izw-berlin.de
Steven Seet (German, English)
Head Science Communication
Tel.: +49 30 5168-125
E-Mail: seet@izw-berlin.de