Taarifa kwa vyombo vya Habari
Chanzo: AFRICA ACADEMY FOR PUBLIC HEALTH(AAPH)
Dar es Salaam| 24-FEB-2024. Wanawake wajawazito nchini Tanzania na nchi nyingine za kipato cha chini na cha kati wanaweza kunufaika na njia rahisi na nafuu zaidi ya kujikinga dhidi ya hatari. Hii ni baada ya utafiti mpya uliofanywa nchini India na Tanzania kupendekeza kuwa kidonge kimoja cha kalsiamu kinachomezwa kila siku kinafaa sawa na vidonge vitatu kwa siku katika kuzuia matatizo kama vile preeclampsia na kujifungua kabla ya wakati.
Preeclampsia ni hali inayosababishwa na shinikizo la damu kuwa juu na protini kuwepo kwenye mkojo wakati wa ujauzito, ambayo inaweza kuwa hatari kwa mama na mtoto. Kuzaliwa kabla ya wakati, kama jina linavyosema, ni kujifungua mtoto kabla ya wiki za 37 za ujauzito. Matatizo yote mawili yanaweza kuwa na athari mbaya, ikiwa ni pamoja na kuongeza hatari ya kifo cha mama, vifo vya watoto wachanga, na matatizo ya muda mrefu ya kiafya kwa mama na mtoto.
Kwa sasa, Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza kuwa wanawake wajawazito wenye ulaji wa chini wa kalsiamu kwenye mlo wao, ambao ni jambo la kawaida katika nchi nyingi za kipato cha chini na cha kati, wachukue miligramu 1500 hadi 2000 za kalsiamu kila siku katika dozi tatu zilizogawanyika. Hata hivyo, utaratibu huu unaweza kuwa changamoto kwa wanawake kuzingatia kutokana na wingi wa vidonge na changamoto za kimfumo za kuvichukua mara kwa mara.
“Matokeo yetu yanaonyesha kuwa kidonge kimoja kwa siku kinaweza kuwa na ufanisi kama vidonge vitatu,” alisema Christopher Sudfeld, mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Harvard Chan, mwandishi wa utafiti huo.
Matokeo haya yalitangazwa Januari 19, 2024 wakati wa Mkutano wa 5 wa Kisayansi wa Mtandao wa ARISE uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania kwa kaulimbiu ya: “Kuziba pengo: Kubadilisha utafiti wa afya na lishe ya vijana kuwa vitendo na sera halisi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara”.
“Nyongeza ya kalsiamu inapaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa mipango ya lishe kwa kiasi kikubwa katika maeneo ambayo inahitajika zaidi—na inapaswa kuanza kuokoa maelfu ya maisha ya mama na watoto wachanga,” anasema Sudfeld, kwa kuzingatia kwamba hii hupunguza idadi ya vidonge kwa wanawake na gharama kwa serikali na programu ambazo hununua vidonge hivi vya kalsiamu.
Matokeo ya utafiti yalitolewa kwa watunga sera, akiwemo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, wabunge wengine wawili, na wadau kutoka CDC Tanzania, Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na mashirika mengine kadhaa ya afya.
Utafiti huu mpya, uliochapishwa Januari 11, 2024 katika The New England Journal of Medicine, ulihusisha wanawake wajawazito zaidi ya 22,000 nchini India na Tanzania. Nusu walipewa utaratibu wa kawaida wa vidonge vitatu, wakati nusu nyingine walipewa kidonge kimoja cha 500mg. Watafiti walifuatilia afya zao katika ujauzito wote na kufuatilia hali ya preeclampsia na kuzaa kabla ya wakati.
Matokeo yalikuwa ya kushangaza, watafiti wanasema. Nchini India na Tanzania, kundi la kidonge kimoja hakikuonyesha tofauti kubwa katika viwango vya preeclampsia ikilinganishwa na kundi la vidonge vitatu. Wakati matokeo ya kuzaa kabla ya wakati yalipingana kati ya nchi hizo mbili, data zote zilizounganishwa hazikuonyesha tofauti yoyote kubwa pia.
Hata hivyo, watafiti wanaonya kuwa utafiti zaidi unahitajika kuthibitisha matokeo haya katika vikundi tofauti vya watu na kuchunguza athari za muda mrefu.
Utafiti huu ulifadhiliwa na Taasisi ya Bill na Melinda Gates, na uliongozwa na Shule ya Afya ya Umma ya Harvard T.H. Chan pamoja na washirika kutoka India na Tanzania. Washirika nchini India walikuwa Taasisi ya St. Johns. Hapa Tanzania, taasisi zilizoshirikiana katika utafiti huu ni pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) na Taasisi ya Afrika ya Kitaaluma kwa Afya ya Jamii (AAPH).
“Utumiaji wa kalsiamu umekuwa mdogo sana katika mazingira mengi, kwa ujumla kwa sababu ya ukubwa wa vidonge, lakini pia gharama kwa mfumo wa afya, kwa sababu ni vidonge vingi vinavyohitajika kutolewa, lakini changamoto za gharama na usafirishaji zinaweza kuwa zinaongeza ugumu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa AAPH Mary Mwanyika wakati wa mkutano huo, akielezea kuwa huu ulikuwa utafiti wa miaka minne lakini kwa sababu ya changamoto za wa janga la UVIKO-19, ulifanyika kwa miaka mitano.
Profesa Andrea Pembe, ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake na aliyekuwa Makamu Mkuu wa MUHAS, aliongoza utafiti huo nchini Tanzania. Akizungumza wakati wa Mkutano wa 5 wa Kisayansi wa Mtandao wa ARISE uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, alipendekeza, “Kuna haja ya kurejea mapendekezo yetu kuhusu nyongeza ya kalsiamu kwa kiwango cha juu, ili kuwawezesha Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea kutekeleza utaratibu matumizi ya nyongeza ya kalsiamu wakati wa ujauzito ili kuzuia pre-eclampsia na kuzaa kabla ya wakati.”
“Haya ndiyo mapendekezo yetu, na tunatarajia taasisi nyingine kama WHO, Wizara ya Afya kuyachukua kwaajili ya utekelezaji,” alisema Profesa Pembe alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya majaribio.
Jinsi ya kupata utafiti huu:
Kwenye jarida la The New England Journal of Medicine (2024). Umeandikwa na Pratibha Dwarkanath, Ph.D., Alfa Muhihi, M.D., M.P.H., Christopher R. Sudfeld, Sc.D., Blair na wenzake Kichwa cha Habari: “Two Randomized Trials of Low-Dose Calcium Supplementation in Pregnancy” Ipate mtandaoni: https://www.nejm.org/doi/full/10.1056/NEJMoa2307212
Kwa mawasiliano zaidi:
Africa Academy of Public Health (AAPH)
Barua Pepe: info@aaph.or.tz
Piga Simu: (+255) 735166105
WhatsApp: (+255) 739166105